
Unalo jibu la changamoto ya mtu mwingine.
Ulizaliwa ili uje kuwa jibu kwa changamoto ya wengine, acha kukaa na kujiona u myonge, hauwezo kitu, hata kama kikawaida unaona kila kitu kimeshindikana, hauelewi kwanini upo duniani.
Elewa kuwa mpaka Mungu kukuumba alikuwa na kusudi na wewe, lipo jambo aliweka uje kulifanya ili uweze saidia wengine, hebu fikiria hata aliyeweza kugundua hata hii intaneti hauoni ni kwa kiasi gani amesaidia hata injili kusambaa kiurahisi? hebu fikiri pia bila huyu mtu kufanya alichoitiwa je wewe ungeweza kusoma hiki nilichoandika hapa wakati huu?
Amka ndugu, ukikaa na kujifikiria na kuongea na wewe mwenyewe na kwa msaada wa Mungu unajua kabisa ni nini unapenda na kufurahia kufanya, kifanye hicho kwa kujiamini ukijua yupo mtu mahali unamsaidia kusogea anapotakiwa kuwa kwa kufanya hilo jambo, unalo jibu la mtu aliye mahali fulani, kataa kuwa sababu ya kuzuia wengine kufika wanapotakiwa kuwa kwa ujinga wako ndugu. Kwa tunaomwamini MUNGU tunajua katika yeye tunaweza yote, na ametuumba kwa kusudi maalumu na tupo duniani ili kuliishi hilo kusudi.
Kuwa jibu kwa changamoto ya mwingine.
Kwanini yule aweze?
Mara nyingi katika maisha yetu inapotokea labda akatakiwa mtu wa kufanya kitu fulani, wengi wetu huwa hatuwi tayari kujitolea au kuwa msitari wa mbele kufanya hilo, tunakuwa wepesi wa kuwapa wengine au kuwaita waje kufanya hilo na mara nyingi kinachosumbua wengi ni kufikiri hawawezi, ndugu yangu kwanini uwe mwepesi kujiona hauwezi na kuamini huyo mwingine anaweza? Kwani yeye ana nini zaidi yako? au yeye Mungu aliyemuumba ni tofauti na wako? Anavuta pumzi tofauti na wewe? Au ni uvivu, uoga unakusumbua? Badilika, jikubali wewe mwenyewe, jiamini kuwa unaweza, usipojikubali wewe nani atakukubali? kama wewe mwenyewe unaona hauwezi, nani ataliona hilo? Badilika, badili namna unavyojichukulia, wewe ni wa thamani sana, unaweza kila kitu maana Mungu ndani yako anaweza mambo yote, badala ya kuwa mwepesi kuhamishia majukumu kwa wengine, fanya wewe mwenyewe kwanza, kushindwa sio kosa, ukishindwa leo, waweza jaribu kesho ukaweza, cha msingi ni ile kujiona kwamba unaweza, kama wengine wanaweza nawe unaweza pia.
Jikubali, unaweza pia.
Pata muda wa kukaa na wewe
Maisha tunayoishi sasa na maendeleo ya teknolojia , tumejikuta tumebanwa sana na mambo mengi ya kujitafuta riziki kiasi cha kukosa muda wa kukaa wenyewe na kupata muda wa kujiongelesha, kujitafuta, ndio hapa kila mtu kwa imani yake, kwa tunaomwamini Kristo Yesu, tunatafuta utambulisho wetu mpya kwake yeye na kuishi huo. Watu wako busy sana muda wote, mara kazi, huku whatsap, huku facebook, huku marafiki, yaani mambo ni mengi kiasi kwamba waweza kukosa kabisa muda wa kuwa wewe, kukaa na wewe, kuongea na kujua nini unataka katika maisha haya, ni wajibu wako wewe mwenyewe kuona umuhimu wa jambo hili na kujiwekea utaratibu ili angalau kila siku au utakapoweza upate walau saa moja au zaidi la kuwa peke yako, kuna wanaoweza kunishangaa kwanini nasema haya, lakini ndugu sasa wewe muda wote upo na shughuli nyingi, hauna muda na wewe mwenyewe unadhani nani atakuwa na wewe, anani atakuthamini, utajijuaje? na usipojijua utakuwaje huyo mtu uliyekusudiwa kuwa na Mungu wako? Maana hapa hakuna muujiza hapa ni lazima wewe ufanye sehemu yako ili mengine yafuate. Kwani huko ambako watu wanashughulika muda wote ni wapi? kwamba hauna muda unaoutumia bila faida? wataka sema muda wote wafanya ya maana? Hebu kuwa mkwelia angalia ratiba yako tena , na weka muda wa kujitafuta, kujua utambulisho wako ili uweze furahia maisha, maana pengine wahangaika kuongozan wengine, utaongozaje wengine wakati mwenyewe hauna muda na wewe? haujijui hata wewe ni nani, hauoni hatari iliyo mbele yako?
Kaa chini , tafuta utambulisho wako, hakuna wa kukuombea ujue hili ni wajibu wako wewe mwenyewe.
Anza sasa
Wengi wetu katika maisha haya, tumejikuta kuna wakati tunashindwa kuanza kufanya baadhi ya mambo kwa wakati sahihi, huenda ni mradi fulani ungependa kuuanzisha, lakini kutokana na maoni ya watu wanaokuzunguka umejikuta haujui uendelee au lini uanze, au wengine watakuambia hauwezi kwa sababu hizi na zile, huenda ni kweli wanachokuambia maana ndivyo wao wanavyoona , na pengine wao walijaribu wakashindwa ndio maana wanadhani wakati wao walipojaribu na kufanikiwa nawe ndipo unaweza kuanza na kufanikiwa, lakini sikia nikuambie ndugu yangu, kumbuka ni wao , si wewe, wao wanaona hivyo, lakini waonavyo sivyo unavyoona wewe, kile kilicho ndani yako kilichokusukuma kuanza huu mradi kinakuambiaje, kilikuambia uanze lini? je kilikuambia uje kutafuta mawazo ya wengine, je hilo wazo ulipolipata lilikuwa halijakamilika? kwanini unataka kutumia watu wa nje kukuamulia cha kufanya? , lini ufanye? , wakati ni wewe mwenye ndoto, unaijua na kuielewa vyema ndoto yako, kama kuna kitu unaona hakipo sawa ni vyema kwa imani yako ukarudi na kukaa na muumba wako maana naamini ndiye anayetuwekea hayo mawazo na ndoto ndani mwetu, hivyo yeye ana majibu na maelekezo yoyote ya maswali tunayokuwa nayo, sisemi kwamba usisikilize maoni ya wengine, sikiliza na penda sana kuona wengine wanasemaje kuhusu kile unafanya lakini usipeperushwe kama upepo na mawazo yao, jua nini unataka kwanza wewe na usitegemee wote kukuelewa, wasikilize, chukua ya kujifunza kisha endelea mbele, hata kama walishindwa wote waliotangulia pengine wewe ndio wa kwanza kushinda ikiwa utachukau hatua sasa.
Anza sasa, wakati ni sasa, usije sema oo nilikuwa na wazo kama lile wakati wenzio washalifanyia kazi.
Hofu haina nguvu
Watu wengi katika maisha yetu wanaumbuliwa sana na hofu au naweza sema uoga, wengi wanafanya mambo ambayo hata mioyo yao inawasuta maana wamefanya bila kupenda bali ni kwa kutimiza matakwa ya watu fulani, huenda ni ofisini unakuta mtu anafanya kitu kisichofaa eti kwa kuwa bos kasema, siamini kwamba kila bosi anachosema au kuniagiza nifanye natakiwa kukifanya, nami kama binadamu nimeumbwa na utashi na Mungu kanijaali akili za kuweza kupambanua mambo, hivyo nina uwezo wa kuona kuwa hili linafaa au halifai hata kama yeye anaona linafaa, naweza kutokufanya na nikamwambia kwanini sifanyi, anaweza akanielewa au asinielewe hilo litakuwa tatizo lake maana sikuumbwa kutaka kila mtu anielewe nilivyo bali jambo la msingi ni mimi kujitambua, kuelewa thamani yangu hili linatosha sana, maana ukijitambua hautaruhusu kusumbuliwa au kupelekeshwa na mwanadamu awaye yeyote, maana unajua hatma yako haipo mikononi mwake , najua kuwa naweza kuendelea hata baada ya pale, najua kuwa sikuzaliwa kuja kuishi ndoto za wengine, ninayo ndoto yangu, sikubali kuendelea kuishi ndoto za watu wengine, hata kama ikinibidi kuishi ndoto za wengine basi ni wakati ambao nipo njiani kuelekea kule ninakotakiwa kuwa na Mungu wangu, kule alikonikusudia niwe tangu aliponiumba, hivyo hofu na uoga havina nafasi kwangu kabisa, maana ninayemwamini kaniambia nisiogope, kasema hakunipa Roho ya hofu, hivyo sioni sababu ya kugopa lolote au mtu yeyote yule maana aliye ndani mwangu ni mkuu kuliko wote wa ulimwenguni hapa, hivyo ninajua kuwa ninaweza kufanya chochote hata kama watu wote hawaniamini au kunikubali, wengine ikibidi watanielewa mbele ya safari , usimuogope mtu anayeweza kuzimika muda wowote, asikufanye ushindwe kufikia ndoto zako, ni mwanadamu tu huyo, si wa milele , yupo leo kesho anaweza asiwepo, hivyo mwamini Mungu kuwa unaweza kila kitu, anakuwezesha yeye, hata ukitishwa usihofu kabisa.
Usiipe hofu ushindi maishani mwako.
Fanya jambo kwa kuwa unafurahia kulifanya
Wengi wetu katika maisha tumejikuta tukiishi maisha yasiyo ya uhalisia, wengi tunaishi kama watu wengine wanataka tuishi, huenda ni marafiki, familia n.k, unakuta mtu anafanya kazi fulani kwa kuwa ni wazazi wake wanataka na kupenda afanye vile lakini yeye hapendi wala kufurahia kazi ile, au mwingine anafanya kazi fulani kwa kuwa ndiyo inayomlipa sana kwa wakati huu, au mwingine anasoma masomo fulani ili aonekane tu naye ana uwezo fulani kwa kuweza kuyamudu. Ndugu yangu haukuzaliwa kuja kuishi maisha ya kufurahisha wengine, ulizaliwa uje uishi wewe kama ulivyokusudiwa na Mungu wako, huenda ni kweli wazazi wamekuchagulia hiyo kazi na ni kwa kuwa wanakutakia mema, lakini haya ni maisha yako na unaishi mara moja tu, hivyo usiishi kwa ajili ay wengine, ishi wewe , ishi kile umeumbiwa kukiishi, fanya kile unapenda maadam una uhakika ndicho amani yako inapatikana ukikifanya, kumheshimu mtu si kuwa mtu wa ndiyo tu, kuna wakati unaweza mwambia hapana na ukamweleza ni kwanini haukubaliani na anachotaka ufanye kwa wakati ule, au pengine ni hiyo kazi unaifanya kwakuwa inalipa sana kwa wakati huu, umewahi fikiria kuwa kuna wakati haitakulipa na je bado utapenda kuifanya hiyo kazi? Ndugu fanya kile unapenda na kufurahia , kile ukifanya moyo wako unakuwa na amani bila kujalisha unapata nini, hela zipo tu na si kila kitu, pengine upo shule unang'ang'ana kusoma masomo magumu ili tu uonekane nawe una akili sana wakati moyoni wala haupendi hayo masomo, wasomea sifa tu, huoni kama ni kujitesa? kwanza ni lazima utumie nguvu nyingi ili uelewe na uweze fanya vizuri maana hicho kitu hakipo damuni na haukipendi ila wafanyia sifa tu, ukipata sifa kitafuata nini?
Acha ujinga, kua , jitambue ndugu haukuzaliwa kuja kufanya ujinga huo
Usisikilize kelele za wasiokufahamu
Ndugu yangu, linda na chunga sana kile unasikia, angalia kama kinaongeza nini kwako, usije kujikuta kutwa unasikiliza watu wenye mtazamo usio sahihi juu ya mambo na wewe ukajikuta unaamini hayo, unakaa na watu ambao muda wote wanakuambia hauwezi, kila unachotaka kufanya wanakuja na sababu kibao za kwanini hauwezi kufanya hicho kitu kwa ufanisi, wengine watakuambia haujui, hauna uzoefu wa kutosha, au watasema subiri mpaka upate mtu wa kukuelekeza au ujifunze kwa waliofanikiwa katika hilo, lakini ndugu yangu, ni kweli haujui lakini utajuaje kama hautafanya hilo? Hata huo uzoefu unaupataje bila kuanzia mahali? hao watu wa kukuelekeza pengine ni mpaka upihe hatua fulani ndio utakutana nao katikati ya safari, inabidi ufanye kile ulichonacho sasa hivi, unacho kitu cha kuanzia, haijalishi unaambiwa nini, ulivyoumbwa uliumbwa na kitu cha kuja kufanya, hauhitaji mtu wa nje kuja kukupa maelekezo namna ya kufanya , fanya kile unasikia toka ndani mwako ilimradi ni kitu chema, hauvunji sheria za nchi wala kuhatarisha maisha ya wengine, fanya, fanya, ukikosea utajifunza wakati upo kwenye mchakati, usisikilize wanaosema utashindwa hata kabla haujaanza, hata kama ukishindwa si tatizo maana hata katika kushindwa yapo ambayo utakuwa umejifunza na ukirudia tena utafanya kwa usahihi zaidi. Kwa tunaomwamini Mungu , tunaamini kuwa hakuna lisilowezekana kwake Mungu, tunayaweza yote katika yeye atutiaye nguvu, hivyo hatuoni kushindwa kabisa maana tunajua hatupo peke yetu, hatufanyi sisi bali yeye aliye ndani mwetun ndiye mwenye kufanya hayo yote kupitia sisi, hivyo nikisema siwezi nakuwa sijielewi, sijui thamani ya aliye ndani mwangu, aliye ndani mwangu anaweza yote, hivyo haijalishi watu wananiambia nini, mimi nasikiliza na kufanya kile Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu ananiambia nifanye, hawezi kunipotosha.
Tambua thamani yako, jikubali na toka hapo uliponasa, songa mbele.
U wa thamani sana
Ndugu yangu , wewe ni wa thamani sana, kipo kitu ndani yako, hakikuwekwa ufe nacho bila kuwafaa watu na jamii inayokuzunguka kwa ujumla. Haijalishi watu wanakuambia nini au wanakuonaje, haijalishi umepotea kiasi gani na pengine umetamkiwa maneno yasiyofaa na ndugu, familia marafiki nk kwamba hauwezi, wewe ni mjinga, haujui kitu, umeshindwa , hauna akili hauwezi fanya lolote, ndugu yangu hayo ni maneno yao na ni maoni yao, ndivyo wanavyoona wao lakini sivyo Mungu anavyokuona, kwake yeye wewe ni mwana upendwaye sana, kipo kitu cha thamani sana ameweka ndani mwako, ni wajibu wako na uamuzi wako kutambua na kukubali kuwa wewe u wa thamani sana, kipo kitu ndani mwako kizuri tu, yani yapo madini ndani mwako ambayo unatakiwa kuruhusu watu wayachimbe yakufaidishwe wewe na wao kwa ujumla, ulizaliwa kuwa suluhu kwa jamii yako, haukuzaliwa kuja kuongeza idadi ya wasiojitambua, walalamishi. Wewe ni wa tofauti , onyesha utofauti wako, ishi kama ulivyokusudiwa uwe, usiishi kama wanavyosema uko, hao ni wanadamu tu hawaoni ya ndani mwako, Mungu wako aliyekuumba anajua u wa thamani sana, hakupoteza muda kukuleta hapa duniani, toka hapo walipokuweka, inuka, nenda ulipokusudiwa na Mungu wako.
Usiruhusu kelele za wasiokuelewa kukupoteza ndugu.
Ulizaliwa kwa kusudi maalumu
Kila mtu aliumbwa kwa kusudi maalumu, acha kuishi ukitamani kuwa kama wengine, unapoteza muda wako bure hauwezi kuwa kama hao, kaa na Mungu wako jitafute, tafuta kujua wewe ni nani, kwanini umezaliwa na ukishajua kwanini upo , kuwa huyo mtu hakuna cha kukuzuia.
Watu wengi tunaishi tukitamani kuwa kama watu fulani kwa kuwa kuna mambo wanafanya tunayapenda, au tunayafurahia, lakini nawe unacho cha thamani kimewekwa ndani mwako, ni wewe wa kukitoa, wapo wanaokisubiria hicho kitu, hakuna wa kuja kukitoa, ni wajibu wako wewe mwenyewe kugundua hicho kitu na kukiishi hicho bila kuangalia mazingira yanasemaje ndugu yangu.
Kama unataka kuishi kwa raha kuwa wewe usitamani wala kutaka kuwa kama wengine, u wa thamani sana.
Give Your Comment
Post a Comment